Sunday, July 21, 2013

Makala-sakata la mkoa Mpya wa songwe,Mbunge Ileje akalishwa katika benchi,wanaileje waweka njama za kuwashambulia Mbunge na Mwenyekiti wa Halmashauri wakidai wamewahujumu,wanahabari nao wawekewa kizuizi,Kigogo mwandamizi serikalini naye apenyeza kwa meseji,Chunya waibuka na kusema makao makuu ya Mkwajuni watanufaika Ileje,Mbozi na Momba,barabara za kukatisha zaingia katika bajeti


Makala-sakata la mkoa Mpya wa songwe,Mbunge Ileje akalishwa katika benchi,wanaileje waweka njama za kuwashambulia Mbunge na Mwenyekiti wa Halmashauri wakidai wamewahujumu,wanahabari nao wawekewa kizuizi,Kigogo mwandamizi serikalini naye apenyeza kwa meseji,Chunya waibuka na kusema makao makuu ya Mkwajuni watanufaika Ileje,Mbozi na Momba,barabara za kukatisha zaingia katika bajeti

Na Thompson Mpanji


SAKATA la mkoa mpya wa Songwe linazidi kuchukuwa sura mpya baada ya Mbunge wa Jimbo la Ileje Aliko Kibona  kukalishwa katika benchi la wakazi Ileje wanaoishi jijini Mbeya  kutoklana na madai ya kuwapeleka wananchi wa Jimbo lake wasikokutaka huku waandishi wa habari wakizuiwa kwa takribani nusu saa na baadaye kuruhusiwa.

Aidha kulikuwepo na taarifa ya kutaka kumfanyia fujo Mbunge huyo  kwa tuhuma za kuwa yeye na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje,Mohamedi Mwala  ndiyo chanzo cha mgogoro wote  huo kutokana na madai ya kukubali mapendekezo ya makao makuu ya mkoa pendekezwa kuwa katika mji wa Mkwajuni,wilayani Chunya.

Hata hivyo mkakati huo uliingia dosari baada ya waandishi wa habari kuingia katika kikao hicho bila matarajio na hivyo wakazi hao kuhofia mchezo huo mchafu kuanikwa na vyombo vya habari  lakini waliwageuzia kibao wanahabari kwa kuwazuia kuingia ndani ya kikao hicho kwa takribani nusu saa  na baadaye kuwaruhusu wakidai kuwa tamko lilishatolewa na waandishi wa habari waliokuwepo wameshalichukuwa na kuondoka na kilichobakia hapo ni wanaileje kujadili mambo yao ya ndani.

Taarifa kutoka ndani ya kikao zilililiambia Mwanahabari kuwa  kulikuwepo na taarifa za Kiongozi mmoja wa ngazi ya juu serikali aliwatumia taarifa wakazi hao kuwa wakati wao wakimngojea Mbunge wao katika kikao hicho amepata taarifa kuwa anafanya mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya Mbeya Peak lakini aliwasihi waendelea na kikao na ajenda zilizopo mezani na kwamba yeye angetarajia kuingia  kwa ndege siku ya Jumamosi(julai,13,2013).

Aidha  jazba waliyokuwa nayo wakazi hao ilishuka baada ya waandishi wa habari kuruhusiwa kuingia katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Kiwira,jijini Mbeya na  kuelezea kile alichozungumza Mbunge wao katika kikao naa waandishi wa habari  katika Hoteli ya Mbeya Peak muda mfupi kabla ya kufika hapo kuwa ni  kupinga makao makuu ya mkoa kwenda Mkwajuni jambo lililowafanya wakazi hao kulipuka kwa furaha na kushusha pumzi nahatimaye  kumkaribisha kwa shangwe kwenda Mheshimiwa Kibona  kukaa katika  'high table' na kuanza kuwahutubbia .


Mbunge huyo anaendelea kusema kuwa wananchi wa Ileje waliposikia suala la Mkoa mpya kuwa Songwe  walijuwa unatokana na mto Songwe  na kwamba hawakuelewa kwamba ilihusishwa na Songwe ya Mkwajuni,katika Jimbo la Songwe,wilayani Chunya kwani walijuwa  lengo la kuchagua jina hilo ni kuuenzi mto songwe uliopita Ileje,Tunduma hadi unaingia Ziwa Nyasa na kutengeneza mpaka wa Tanzania na Malawi,na kwamba mto huo unapita kuzigusa Wilaya za Mbozi,Ileje na
Mbeya vijijini na hakukuwa na uhusiano wowote na Jimbo la Songwe.


CHANZO CHA MVUTANO

Mbunge Kibona anasema, "Wananchi wa Wilaya ya Ileje wameshtushwa sana na maamuzi ya RCC kwamba Mkoa mpya unaanzishwa utaitwa Mkoa  wa Songwe na makao makuu yatakuwa Mkwajuni, hapo ndiyo pameleta matatizo wao walipendekeza makao makuu yawe popote katika Wilaya ya Mbozi na hasa Kijiji cha Ezya ambayo kwao ingekuwa ni ukombozi kutoka wilayani kufika makao makuu ya
Wilaya  kupata huduma na  waliona ndoto zao zingekomboka.

"Wananchi wote wa Ileje wanaoishi popote nchini  watambue kuwa  wazazi wao hawajakubaliana  na masharti ya
kuanzishwa Mkoa  ni magumu kufikia watu idadi ya milioni na hivyo wanasema wameburuzwa  na kwamba wakati umefika wa kuhitaji
ukombozi wao,wanasema  tutafanya kazi kwa kushirikiana na serikali,tutalima tutakavyoweza tutafanya kazi za maendeleo kadri
tutakavyoweza  lakini suala  la Mkwajuni hapana hawapo tayari  nami naungana nao walikuwa wakitembea kilomita 160  hadi mjini Mbeya
na sasa wameongezewa tena  kilimota 90 za kwenda Mkwajuni suala hili linamadhara kiuchumi,kisiasa na pia kijamii,"alifafanua.


Kijamii.

Mbunge Kibona amebainisha kuwa mapendekezo hayo yameibua mahusiano mabaya  na chuki imejengeka kati ya serikali
na wananchi wa Ileje kutokana na kuingizwa siasa na watu  ambao siyo wanaccm wanasema sera yao siyo kuanzisha mikoa mipya
bali ni kusogeza huduma karibu na wananchi  na kwamba kinachotakiwa  kufanyika ni yale mambo yanayotakiwa yapatikane mikoani yapatikane katika halmashauri na hivyo  wananchi kushawishika na wameshashika bango  na hatimaye kuna pengo  limeanza kujitokeza kati ya serikali,ccm na wananchi wa Ileje kuanza kuyumba.

"Na mimi kama ambaye ninawakilisha Wilaya mwakilishi wa Ileje sipo tayari  kuona  mambo hayo yanatokea kuona Wilaya yenye utulivu kuliko zote kwa muda mrefu inaanza kugombana na serikali sipo tayari na serikali iangalie jambo hili kungali mapema hata bila kusubiri hatua zingine zambele,"alisema.


Kiuchumi
Mheshimiwa Kibona amesema  ili mwananchi aende kupata huduma katika makao makuu ya Mkoa wa Mbeya alikuwa akiuza Kuku wawili
na sasa atalazimika kuuza kuku  watano  hadi sita  ili afike Makao makuu mkoa mpya wa songwe,"Mkwajuni na hasa ukiwakadiria wananchi wa kutoka  Luswiswi,Bulanga,Ndondela,Ikinga,Mgaya,Kapeta apande basi kwenda boda,aende Kyela hadi Uyole akifika Mbalizi  anakuta magari yameondoka alale aende kesho
Mkwajuni,wazazi wetu  Ileje wamesema ili hapana."



Kisiasa

Kibona amesema amekuwa akipokea  meseji  kutoka kwa  wananchi Ileje kupitia simu yake ya kiganjani  wakisema endapo pendekezo la sekretarieti litapitishwa  basi Chama cha Mapinduzi wilayani Ileje kitakuwa hakina nafasi  katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 jambo ambalo amepinga vikali akidai CCM ndicho chama kilichomweka madarakani na yeye hayupo tayari kianguke kwani sera ya chama ni  pamoja na kuwasikiliza  na kuwasaidia wananchi sanjari na kuwasogezea huduma
jirani.

"Hiki ninachokisema nimetumwa na wazee wa Ileje na mimi kama mwakilishi wao nawaunga mkono na hivyo kwa niaba ya wananchi wa Ileje tunasema  ni bora tukaenda Malawi kuliko kwenda Mkwajuni na nimekuwa nikitumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kutoka kwa wanaileje waliopo wilayani Ileje,nje ya Ileje,mkoa wa Mbeya na mikoa mbalimbali tanzania  wakiniambia kuwa kama maamuzi hayo hayatabadilishwa CCM bai bai Ileje,"alisema.


"Tukumbuke Baba wa Taifa alianzisha Vijiji vya ujamaa nami nikiwa mtu mzima nilisikia hoja iliyokuwepo alisema hawezi kuwahudumia watu wake wakiwa mbali wakiwa jirani atawasogezea Shule,maji,Hospitali  na wananchi wa Momba,Mbozi na Ileje wapo jirani tayari wamejimobilize
pamoja,"alisema .


Aliongeza, "haiwezekani wananchi zaidi ya 800,000  uwaambie kuwa sitowapa huduma  hapa mlipo
huduma yenu mtaifuata kwa watu 200,000 wananchi wa Ileje,Momba na Mbozi
katika vikao vya awali tumeliona jambo hili lina athari kwa CCM na dola yetu,ni muda muafaka sasa  wa kutangaza kuwa
hili jambo halijakubalika."


Mbunge huyo alisema anafahamu  suala la kuanzisha mchakato Mkoa  una sheria yake ambayo  inasema Rais atatangaza nia
ya kuanzisha maeneo mapya ya Mkoa na kutangaza kuwa wale wenye mawazo wapeleke,na kwamba wao  wanasema ikifika huko  kwa
Rais itakuwa makosa  kwa pendekezo kwamba makao makuu yawe  mkwajuni hivyo ni vizuri wakasema bado  mapema ili Mheshimiwa Kikwete alifahamu.



Ileje na Malawi.

Akizungumza katika kikao hicho huku akishangiliwa na wakazi hao Mbunge Kibona  ametoa tamko la wakazi wa jimbo la Ileje kuwa
wanakubaliana na maamuzi yaliyofikiwa na kamati ya ushauri ya Mkoa wa Mbeya  kuhusu mapendekezo ya kuanzishwa mkoa mpya
Songwe  lakini hawapo tayari  kwenda katika makao makuu ya mkoa mpya pendekezwa katika mji mdogo wa Mkwajuni wilayani Chunya na kwamba ni
bora waende nchini Malawi walikokuwa wakipata huduma kwa urahisi za matibabu tangu miaka ya 70.


Alisema kuwa  katika kipindi chote tangu miaka ya 70 hawakuwahi kupata huduma ya afya  kutoka serikali ya Tanzania na  kwa nafasi ya pekee wanaishukuru serikali ya Malawi kwa kuwapokea kuwahudumia bure kwa  tiba na wagonjwa waliofariki dunia wakiwa katika Hospitali ya Chitipa na Chinunga  miili yao ilisafirishwa  kwa kutumia magari ya  serikali ya Malawi  hadi mpakani mwa Tanzania na Malawi.



Sekretarieti

Mbunge huyo anasema uzoefu unaonesha kuwa  hata katika vikao vya Bunge wamekuwa wakipiga kelele kugombana na mawaziri kwa
sababu ya kupotoshwa na sekretarieti, na wakati mwingine wamekuwa wakipokea kitabu cha bajeti inaonesha  wilaya yingine shule
zitakazokarabatiwa ni  shule 30  huku kukiwa hakuna tofauti unakuta wilaya nyingine  imetengwa bajeti ya shule nne.

"Unakuta Waziri alikuwa na nia nzuri lakini aliyepotosha ni sekretarieti,kuanzia makatibu wakuu, wakurugenzi na wakurugenzi wa halmashauri  na  mikoani
watu wanawanyooshea vidole watendaji uenda hawakitakii mema Chama cha Mapinduzi  kwa sababu haiwezekani mimi naamini wanampotosha RC kwa sababu haiingii akilini kutoka Ileje hadi Mkwajuni 'nikirefer' kutoka vijijini bado  wengine wanatembelea kwa kilomita zaidi ya 200 leo wananchi unawapeleka mbali zaidi eti umewasogezea huduma,"alisema.

Anaongeza Mbunge huyo,Mimi nadhani hapo mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na sekretarieti yake  kama hawakufanya kwa makusudi basi kwa bahati mbaya sana,hivyo kuna haja ya kurejea  upya hayo maamuzi,na ametoa wito kwa wananchi wa ndani na nje ya Ileje ambao wamemtumia ujumbe mfupi wa maandishi  kuhusu mikakati yao ya kutaka kuandamana kulala barabarani kwenda kwa Mkuu wa Mkoa, wasifikiea uamuzi huo  kwani  vikao vingi vizito vimekwishafanyika na hivyo wasifikiea hatua ya kupewa sifa mbaya.

"Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni sikivu ninaamini wadau wengi kama nilivyosema mbozi wanalia,Momba
wanalia,leo (julai,12,2013) tumefikia kikao cha pamoja,tumefikia maazimio ndugu
zangu wanaileje mliopo popote nchini naomba muwe watulivu baada ya kauli hii ni
kwa niaba ya wazazi wenu walioko Ileje tuwache mawazo ya kufanya fujo
kumkashifu,kumtukana mtu yeyote si vizuri badala yake tuendelee kujadili na
tutoe mawazo ingawa muda wa kutoa mawazo haujafika kwa sababu mawazo haya mapendekezo
haya yakifika  kwa Rais atatoa tangazo la kusudio la kuanzisha makao mpya hapo ndipo atakaribisha maoni kutoka kwa wadau
kutoa maoni, kwa sasa hekima itawale na busara itawale,"alisisitiza.


Anasema  wao wameathirika kwa kiwango kikubwa Momba,Mbozi na Ileje kwani hata katika michakato yao hawakupendekeza kwenda
Mkwajuni na wala Chunya haikupendekeza  makao makuu yawe Mkwajuni  isipokuwa sekretarieti ndiyo imeuza  jambo  hilo na kwamba  watu wamediriki
kusema kuwa sekreterieti  inataka CCM isambaratike  kuelekea 2015,"mgogoro wa kisiasa unaingia kama nilivyosema lakini
tunakwenda kuudhibiti kwa kujenga hoja."


Kuanzisha bifu na Mulugo

Mbunge Kibona anasema,"tunachozungumza
ni hoja,ningekuja na hoja ambazo hazina mashiko ninyi mgeanza kunicheka,lakini niwaambie wanahabari katika
wabunge wa Mkoa wa Mbeya Mulugo nipo naye karibu sana na mimi nina "declare
interest" ni rafiki yangu sana lakini  tukikaa hapa tutazungumzia hoja kwani  ukaribu wake
mimi haunizuii  mimi kuleta mawazo ya watu wa Ileje."

Alisema jambo hili linahitaji kuchukuwa muda mrefu kulitafakari  ingawa alisisitiza kuwa hajatangaza  mgogoro na
Mulugo  isipokuwa mulugo kibinadamu lazima  ataona kwamba sasa
mambo haya hayaendi vizuri,lakini ni lazima hawahurumie  wananchi wa Ileje.


Mbunge kibona akana kuburuzwa na wabunge wenye majina

"Maamuzi haya huwezi kukwepa siasa ,kwa sababu ndiyo inasema
tusogeze  huduma kwa wananchi,siasa inasema tusogeze huduma kwa wananchi na
ndiyo ipo katika ilani ya uchaguzi kwa sababu
ndiyo inasema kila kijiji kitakuwa na vituo vya afya kila kata itakuwa na  vituo vya
afya lakini vijiji na kata zingine hakuna huduma hizo,jambo hili hauwezi
kulitofautisha ama kulitenganisha na siasa kwa sababu siasa ndiyo maisha yenyewe



"Sijaburuzwa na mtu na sitegemei kuburuzwa na ndiyo maana nimekuja hapa bila kupata ushauri kwa  mtu kuhofia fulani atanielewaje  mimi nipo tayari kuburuzwa na wananchi wangu  wapiga kura na wakiniambia geuka kushoto nitageuka nikishageuka nitajenga hoja na nitasema huku mlikosema nigeukie  ndiko linakotokea  vumbi mnaonaje nigeukie ambako vumbi halitokei wakikubaliana na hoja yangu nitageukia upande mwingine lakini si mtu mwingine lakini akiniambia jambo la msingi lenye hoja nitalikubali hili la kuweka makao makuu badala ya mbeya ninaliona halina mashiko,vikongwe,vijana wadogo wananiuliza kila
ninapopita eti mnatupeleka wapi huko nendeni  wenyewe,"aliendelea kufafanua.



Hofu ya Elimu kwenda Rungwe

"Wataalamu wanasema  katika maisha  yako yote jitahidi sana kufanya maongezi na mtu
aliyekuzidi,husifanye na mtu ambaye yupo sawa na wewe mtafute anayekuzidi
ustaraabu,elimu,kipato hili ujifunze kutoka kwake , suala la kukimbia siyo hoja kwa
sababu ni wapiga kura wangu  lakini wasingekuwa ni wapiga kura wangu ningetumia maneno mazito  kuliko
hili,niseme kuwa wananchi wangu hawakufahamu lakini  wakifahamishwa wataelewa,
fanya urafiki na maongezi kwa mtu anayekuzidi,kwa sababu ukifanya urafiki na masikini hautapata chochote,"alifafanua.


Hata hivyo Mheshimiwa Kibona alikiri  kuwa histori ilikuwa inaonesha  zamani wananchi wa Rungwe kwa asilimia kubwa waliwazidi kielimu  lakini kwa sasa wanakwenda  na kusonga mbele hivyo hawahofii kuwa nao pamoja  ambapo kuhusu suala la  wananchi wa Ileje kutumikishwa amelikanusha  akidai walikuwa wanawasingizia  wenyeji  wa kabila la wandali na kwamba ukweli ni kuwa wanawake wa kabila la wandali walikuwa wakitumwa na wandali wenzao waliokuwa wakimiliki maduka kwenda kuchukuwa  chumvi  na hasa akina mama sanjari na sabuni,mafuta ya taa majola ya nguo  wilayani Rungwe,kwani wananchi wa kabila la kinyakyusa hawakuwa na
maduka Ileje.



Muda siyo muafaka kupata mkoa.

Mbunge huyo anahitimisha kwa kusema Sekretarieti imewaweka njia panda,wananchi wa ileje
wanasema kama ombi lao halitapokelewa wanadhani muda siyo muafaka kuunda Mkoa
Mkoa lisitishwe na kuja kujadiliwa  wakati utakaporuhusu maana kuna dalili za kuleta
mafarakano kujenga chuki,"tuache kwanza  kwa maana ukijaribu maji  ukiyaona
ni ya moto  ni vizuri ukayaacha yapoe kwanza na hiyo maana yake  ni kuahirisha
lakini kama litaendelea mwandishi  utakuja kukumbuka ninayosema hili jambo limekuja vibaya,sura
yake mbaya  kwa serikali na watendaji  tukienda kichwa kichwa tutainua kitu ambacho tutajutia."

Mwenyekiti wa Halmashauri Ileje awashukia wananchi

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje,Mohamed Mwala  alisema mtu mwenye mapenzi ya dhati kama kweli inamuuma angekwenda kuonana na na viongozi na wananchi wenzao wa Ileje badala ya kuanza kuanzisha vikao  vyao na kuanza kuwatuhumu  wakati hawajuwi walichokifanya ndani ya RCC ama walitaka kusikia  kuwa wamepigana ngumi ndiyo wangefurahi.

"Siwezi kushughulika na kikao ambacho kipo nje ya utaratibu  sijaandikiwa barua ya kuitwa... hayo  anayoshughulika Mbunge ni ya kwake hayo mambo siwezi kuyatambua ,mimi kama kiongozi napaswa  niheshimiwe siwezi kuwa kiongozi wa kuchezewa kiasi hicho  lazima nijiamini kama kiongozi katika nafasi yangu eti sababu  ni mwanaileje anakaa huko (Mbeya)anajiamulia kujisema, isije kuwa ni watu wa vyama vya upinzani  wanajikusanya  kuunda nguvu wakasema wanaileje,mimi kiongozi niliyedhaminiwa nastahili kuheshimiwa  kama  mimi ninavyowaheshimu wananchi wangu,"alisema Mheshimiwa Mwala.

Mheshimiwa Mwala  alisema haiwezekani ukawalalamikia watu  nje ya nyumbani  badala ya kufika kuona makubwa wanayoyafanya viongozi na wananchi hao,"hatuwezi kuongoza wananchi  huku wengine wanasema hivi, huku wengine wanasema vile,tulinyoosha mikono tukazungumza lakini demokrasia ilitumika wengi walishinda au walitaka waoneshwe katika vyombo vya habari kama mwala na Mbunge walipinga,unajuwa mwandishi mkataa kwao ni mtumwa,hauwezi kupata baraka kama unaongelea huko nje,jana( julai,11,2013) alikuja Mkuu wa Mkoa Kandoro  walijuwa amekujaje huku na  amesemaje,hatuwezi kuongoza wananchi kwa staili hiyo kwa sababu hatuwezi kuongoza vikao vya wanaileje  leo Mbeya,kesho Iringa."

Mwenyekiti huyo wa Halamshauri ya Ileje alihitimisha kwa kusema kuwa endapo watawaongoza wananchi kwa mfumo huo  watatuyumbishwa na kwamba ameshtushwa kuambiwa kuwa waliokaa na kuwatupia lawama ni wanaileje jambo ambalo  aliendelea kulipinga na kudai kuwa wanaileje hawawezi kuwa na tabia ya kuwatuhumu viongozi wao  kwani siyo asili yao na hivyo wanapaswa kuwa makini katika suala hili kwa upande wa upinzani kujipenyeza.



Wanaileje

Said Ngondo,Mkazi wa Bwipa anayeishi jijini Mbeya ni Mwenyekiti
wa kamati wa wanaileje wazalendo  wametoa tamko kuhusu makao makuu ya mkoa mpya wa Songwe kuwepo mkwajuni kwamba wanapinga
vikali kwenda huko huko.


Ngondo alisema sababu za msingi kutokana na lengo la kusogeza huduma za
msingi kwa jamii hazipo  na matokeo yake wanasogezewa mbali zaidi huduma  na zinaenda kuwatesa wananchi wa
Ileje kutoka vijiji vya kapeta,Mgaya,Ikinga na Bwipa  kwani siyo rahisi kufika katika  makao makuu ya Mkwajuni.


Mwenyekiti huyo amesema hawapo  tayari kwa namna yeyote kupelekwa katika makao makuu ya mkoa ya
mkwajuni na wamependekeza  makao makuu yawe Wilaya ya Mbozi "endapo  sekretarieti itang'anga'nia mapendekezo yao  hatupo tayari katika maamuzi,
na kwa sababu  tupo mpakani ni bora tuungane na Malawi endapo watatumia nguvu  hatulilii maslhi ya watu wachache bali tunawalilia wanaileje wote hata wazee wetu wasio na elimu wanatuuliza kama tunazo  akili timamu,tunasema hata katika shughuli za maendeleo hatutashiriki."

Mgombea ubunge wa Jimbo la Mbeya mjini

Eugen Kisonga almaarufu Tk amesema mgao wa Mkoa mpya wa Songwe umezingatia
jiografia ya Wilaya  kwani Wilaya karibu zote katika kilimo cha kahawa,Tumbaku,Mpunga ,madini katika Wilaya ya Chunya na Ileje  wanafanana kwa mengi na kwamba Mkwajuni kuwa  makao makuu  ni sahihi  kwani kuweka makao makuu wilayani Mbozi,Ileje ama Momba kiusalama  ingekuwa hatari kutokana na kupakana na mpaka wa Malawi na  Zambia


Mgombea huyo wa Ubunge kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 Kisonga anasema Chunya ni kubwa sana hivyo pia kimawasiliano inatendewa haki kwani ni rahisi  kufika mkwajuni kutoka Ileje kuliko sehemu nyingine yeyote ile ya chunya inayopakana karibu na mikoa
minne, na hivyo ameupongeza uamuzi  wa wa sekretarieti ya Mkoa wa Mbeya kuwa ni wa  busara  kwa maana suala  la ukabila ,udini  au umaarufu wa baadhi ya Wilaya  ama watu halikuzingatiwa, uamuzi ulipitishwa na vikao vya madiwani mkoa mzima ingawa unaonekana ubinafsi ulitawala  kwa madiwani kutetea  baadhi ya maeneo yao.

Mwenyekiti wa CCM/Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya

Akizungumzia suala hilo,Mheshimiwa Kapala Makelele ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya amesikitishwa na suala hili  kupotoshwa  huku akiwashangaa viongozi ambao walikuwa wajumbe wakati mapendekezo hayo yakipitishwa  katika kikao halali na kikubwa cha kamati ya ushauri ya Mkoa  na kugeuka baada ya kufika kwa wananchi.

"Viongozi tunatakiwa kuwa na msimamo kwa sababu yanayopitishwa na vikao halali yanapaswa kuheshimiwa,kwa sababu suala  la Mkoa mpya lilianzia mchakato katika vikao vya baraza la madiwani na kamati za siasa na baadaye  baada ya kufika RCC ziliangaliwa hoja na hatimaye kupitishwa,sasa leo iweje kiongozi yule yule aliyekubali maamuzi hayo ageuke na kupinga tena,demokarsia ilitumika sasa iweje mtu anatoka nje ya kikao anabadilika?,"alihoji Mheshimiwa Makelele.

Makao makuu ya Mkwajuni, Ileje,Mbozi na Momba kunufaika kwa ukaribu

Mwenyekiti huyo alisema endapo mapendekezo hayo yatapitishwa makao makuu ya Mkoa wa Songwe kuwa Mkwajuni kutakuwa na umbali mfupi kwa wanannchi wa Wilaya ya Ileje na Momba ambao kwa sasa wapo mbali na makao makuu ya Mkoa wa Mbeya kutokana na kufunguliwa njia mpya za mkato kuliko kutumia njia ya Mbalizi.

"Unajuwa njia zitakazotumika  baada ya kukubalika wazo la makao makuu kuwa Mkwajuni ni hii ya kupitia Garula,magamba ya Chunya na kutokea  Magamba ya Mbozi na Itindi ambayo ni fupi sana  na kwenda Momba kuna njia ya kupita Garula  hadi Mheza barabara ambayo tayari ipo katika bajeti ya mwaka  huu kwa hiyo  watu wa Ileje watajikuta wanatumia masaa mawili hadi moja hadi kufika makao makuu ya Mkwajuni alikadhalika na Momba na Mbozi...lakini hata hayati Baba wa taifa aliamua makao makuu ya Nchi yawe Dodoma ilikuwa ni porini lakini sasa watu wamekwenda na unaonekana ni mji kwa sababu ulinzishwa kwa lengo maalum na hivyo sasa unaendelea kujengwa kimpangilio,"alifafanua.

Diwani wa Mkwajuni ataja barabara za Mkoa wa Songwe ni fupi kuliko kwenda Mbeya mjini

Naye Diwani wa Kata ya Mkwajuni Chesco Ngairo amepongeza maamuzi ya RCC Mbeya na kusema yamelenga kumkomboa  mtanzania aliyeoko mbali na huduma muhimu za kijamii ikiwemo na huduma za kiutawala bila kujali idadi ya watu  ama uwezo  huku akirejea maisha ya watu wa Ngawala,Ngua,Udinde Rukwa na Kambikatoto ambao hadi  kuzifikia huduma za kijamii endapo makao makuu yatakuwepo Mkwajuni watatembea umbali wa zaidi ya kilimota 230 tofauti na mtu wa Ileje ambaye atatembea umbali wa takribani kilomita 70 hadi 80.

"Unajuwa endapo Makao makuu ya Mkoa mpya yatakuwa Mkwajuni,mwananchi wa Ileje kwa kutumia njia ya Garula,Magamba atatumia muda mfupi kufika Mkwajuni  kutokana na kutumia kilomita takribani 70 ama 80 kuliko wa kambi katoto  ambaye atatumia zaidi ya kilimota 230 na mtu wa Ngwala,Gua na udinde Rukwa atakayetumia kilomita zaidi ya 180,kwa hiyo ndugu zetu wasitumie kampeni chafu kwa makusudi bila hoja za msingi,watuonee huduma serikali imeliona jambo hili kwa macho mawili,"alisema Diwani Ngailo.

Mwisho.