Saturday, September 10, 2011

Na Thompson Mpanji HIVI karibuni kumetokea habari za kusikitisha zisizokuwa za kawaida ambapo wakulima na wafugaji wa Kitongoji cha Tagawanu,Kijiji cha Ikanutwa,Wilaya ya Mbarali,mkoani Mbeya kuhusu dhamira yao ya kuwaburuza mahakamani Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa hifadhi ya taifa (TANAPA) kutokana na kupunjwa haki zao za malipo ya fidia ya mashamba na nyumba. Wanakijiji hao wamesema tayari wameshamuona Mwanasheria,Bw.Victor Mkumbe wa jijini Mbeya kuomba ushauri wa kisheria na kwamba wakurugenzi hao wameshaandikiwa notisi ya siku 30 kulipa madai ya wananchi hao haraka iwezekanavyo na endapo utapita muda huo watafikishwa mahakamani kujibu madai hayo. Taarifa za wananchi hao zimemgusa kila mmoja na kuhoji kulikoni serikali iwafanyie dhuruma wananchi wake kiasi hicho na kufikia hatua ya kupuuza madai yao ambayo wanadai waliyatoa awali kabla ya zoezi la kuanza kulipwa hundi ambazo zinadaiwa hazikidhi hata mlo wa siku moja kwa baadhi ya familia hizo. Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti kuhusu kukatishwa tamaa na kutokuwa na imani na serikali baada ya kuyapuuza malalamiko yao ya kupunjwa fidia ya malipo ya makazi na mashamba baada ya kutii amri ya kupisha upanuzi wa hifadhi ya taifa ya Ruaha wananchi hao walisema serikali sasa imeamua kuonesha makucha ya ufisadi kwao bila soni. Huku wakionekana kukataa tamaa na kujawa na jazba wananchi hao walisema kuwa sababu zinazopelekea kukosa imani na serikali ni kutokana na kutosikilizwa malalamiko yao na kwamba maeneo mengi hayakufanyiwa zoezi la uthaminishaji na badala yake wameletewa hundi za malipo ambazo hawajaelewa kigezo kilichotumika. Mmoja wa wakulima hao aliyejitambulisha kwa jina la Bw.Victor Tandika anasema kuwa walishangaa badala ya kusikilizwa malalamiko hayo wameletewa hundi mei,29 mwaka huu ambazo malipo yake hayalingani na mali zao jambo ambalo wameona serikali imedhamiria kuwabagua na kuwanyanyasa na hivyo kujiona kama wakimbizi ndani ya Nchi yao. Mwanakijiji huyo anadiriki kusema kwa uchungu kuwa kama serikali inaona jamii ya wafugaji wa kabila la kisukuma siyo watanzania basi wawaeleze wazi na kuwaonyesha uraia wao na nchi ya kwenda kuliko kuwanyanya,kuwatesa na kuwanyima haki zao halali za msingi. Mkulima mwingine Bw.Silasi Shija anasema kuwa hasira yao imepanda zaidi wakikumbuka namna serikali isivyowathamini ambapo mwaka 2006/2007 Rais alipoteua tume ya jaji Othman kuchunguza malalamiko yao jinsi walivyotendewa unyama wakati wa zoezi la kuhamisha mifugo lakini hadi leo hakuna taarifa yeyote ya matokeo ya tume hiyo na badala yake wanafukuzwa katika makazi yao kama mbwa. Anasema kama hiyo haitoshi wameamrishwa wahame kupisha upanuzi wa hifadhi ya TANAPA jambo ambalo hawajakaidi lakini katika hatua ya kushangaza pamoja na kulalamikia kutokuwepo haki katika zoezi la kufanya uthaminishaji wa mashamba na nyumba sanjari na maeneo mengine kutofikiwa kabisa wamepuuzwa na kupewa hundi ambazo hazilingani na mali zao. Aidha Mkulima aliyejitambulisha kwa jina la Noge Maona anasema kuwa katika zoezi hilo la kuwahamaisha hakuna hata tone la huruma na haki jambo linalopelekea kuhoji ipo wapi dhana ya utawala bora ambayo wanaona kama ni kiini macho kwa wakulima na wafugaji wa maeneo hayo. Mwenyekiti wa kitongoji cha Tagawanu,Bw.Samson Seba anasema zoezi hilo limeibuka ambapo wananchi hawakushirikishwa,hawajaonyeshwa eneo mbadala la kwenda kuishi wala mashamba ya kulima zaidi ya kupewa amri kuhama kaya zaidi ya 512 za wananchi wa kitongoji hicho. Bw.Seba anasema taarifa isiyo rasmi wamesikia wanatakiwa kuhama mwezi huu wa julai ama mapema mwezi agosti na amedai kuwa wanasikitika na hatua hiyo ya serikali kupuuza madai yao na badala yake kuwa chanzo cha dalili za kukosekana kwa amani Aidha anasema kuwa sababu za kukosekana amani na kupelekea migogoro katika nchi za jirani imetokana na viongozi kushindwa kutatua kero na malalamiko ya kabila ama kundi fulani na hivyo kuzua mapigano na hata kuchinjana na kwamba kama Tanzania ni kisiwa cha amani hawatarajii ifikie katika hatua hiyo. Ninachokuwa najiuliza serikali inayasikia malalamiko ya wananchi wake na kama inayasikia kuna lipi ambalo tayari imelifanya katika kuhakikisha kero na malalamiko kama hayo yanakwisha kabisa na wananchi wakabakia na amani na imani na serikali yao. Kama malalamiko ya hawa wakulima ni ya kweli basi serikali imeamua kufanya ubabe kwa kutumia nguvu ya dola kuwaondoa wananchi wake watake wasitake na kama ni hivyo nini basi mwisho wake kama siyo kufikia hatua ya inzi kufia katika kidonda ingawa hatuombei kufikia huko lakini tunaamini kuwa jambo lolote ni bora kulikinga badala ya kusubiri liharibike ndipo jitihada za kulitibu zikatokea. Mara nyingi nimekuwa nikijiuliza hivi staili ya baadhi ya watu kujitokeza katika misiba na kujionesha ‘wanazo’ wakati mtu ameshafariki kwa kutoa rambi rambi ama sadaka maelfu ili watu wamuone kuwa anao uwezo ambapo ukirudi nyuma kuulizia historia ya kifo cha marehemu ni ugonjwa ambao ungeweza kutibika kwa sh.20,000 ama pengine ni njaa iliyomuua marehemu kutokana na kutumia madawa makali,je hao wanaotoa maelfu ya mapesa katika sadaka kama wangeweza kumsaidia mtu huyo asingeweza kupona?, ni sawa na msemo huo,vema kukinga kuliko kutibu. Mimi sitegemei wala sitarajii hata kidogo kama ufisadi unaweza kuhamia kwa wananchi na huku viongozi wa ngazi za juu serikalini wakawa wanasikia vilio vya watu wanaofisadiwa huku wao wakanyamaza bila kukemea wala kuchukua hatua yeyeote zaidi ya kukaa katika mashangangi ya walipa kodi hao hao wakiwa hawana hofu, hainiingii akilini hata kidogo hivi kweli hata juisi ama maji yanaweza yakashuka kooni kweli. Inaweza kufikia hatua ya watanzania kujiuliza hivi viongozi tulio waweka madarakani ni watanzania wenzetu kweli ama ni wakimbizi lakini pia mtu unaweza kujiuliza inawezekana ile dhana inayosemwa mitaani ya ‘Chukua Chako Mapema’ ndiyo imeanza kujitokeza na kuota mizizi?, sipati picha hata kidogo. Mimi nadhani imefika wakati wa serikali kuu kujaribu kuingilia kati, kufuatilia kwa kina vilio vya wananchi wake kujua kama kuna ukweli na ikibidi kutatua kero hizo haraka iwezekanavyo ili kuendelea kujenga imani miongoni mwa watu wake ambayo imepotea kutokana na kuibua kwa vitendo vya ufisadi,rushwa na kashfa kadha wa kadhaa ambazo zimeikumba serikali kupitia viongozi wake waandamizi. Viongozi waliopo huko juu wakumbuke kuwa cheo ni dhamana na hiyo ni dhamana waliyopewa na watanzania ambao leo wanalalamika wanaumi huku wao wamekaa kimya nini madhumuni yao?,watanzania wanaonesha wazi kukerwa na unyanyasaji,dhuruma na unyonyaji na ndiyo maana tukirejea katika historia ya mababu zetu enzi za ukoloni walikubali kufa kwa ajili ya kutetea nchi yao kwa kupambana na wazungu waliokuwa na silaha za moto huku wao wakiwa na malungu,mapanga,mawe,mikuki na mishale lakini hadi walifanikiwa pamoja na unyonge wao. Hatutaki na wala hatuhitaji hayo yatokee kwetu,mifano iliyo hai tunaiona kwa majirani zetu ilianzia kwa majirani wa ukanda wa maziwa makuu lakini tumeshuhudia kwa macho yetu kwa maswahiba wetu Kenya na huko Zimbabwe. Ninachotaka kusema kama kuna viongozi wenye mawazo ya namna hiyo hatuwahitaji hata kidogo ni bora wajihudhuru wawaachie wazalendo wenyemoyo wa huruma na uchungu na nchi yao waweze kuiongoza nchi kwa haki,usawa na amani kuliko dalili zinavyojionesha kuwa kuna baadhi ya viongozi wapo madarakani kwa maslahi yao binafsi na kwamba hata kama nchi ikinuka machafuko watapanda ndege na kwenda kuishi huko ughaibuni na familia zao huku wakiwa wametuachia dhahama,nasema viongozi wa mfano huo wajihudhuru. Kwa ujumla hali ya wakulima na wafugaji wa Mbarali siyo shwari kwa maana mtazamo na maongezi yao unaonesha kila dalili za kuchanganyikiwa na kukata tama hadi kufikia hatua ya kuhoji kama wao siyo raia wa Tanzania basi wanaiomba serikali iwapeleke kule wanakoona ndiyo kwao kwa madai kuwa vilio vyao vinapuuzwa na hawaoni mahali pa kukimbilia kupeleka kilio chao,kama baadhi yao walivyodiriki kusema wanajiona kama wakimbizi ndani ya nchi yao. Kwa hiyo basi ni rai yangu kuiomba serikali kupitia viongozi wakuu wa nchi kufika kuwasikiliza wananchi hao na kufuatilia kwa ukaribu kujua malalamiko yao na kama kuna ukweli basi viongozi wanaohusika ama waliohusika kuichafua serikali kwa maslahi yao binafsi wawajibishwe ili iwe fundisho kwa baadhi ya viongozi wengine wenye tabia kama hiyo,alamsiki. Mwisho